,

Vijana Wa Tume Quotes

Quotes tagged as "vijana-wa-tume" Showing 1-12 of 12
Enock Maregesi
“Saa nane za usiku timu nzima ya Vijana wa Tume ilirudi San Ángel katika helikopta ya DEA, tayari kwa safari ya Salina Cruz katika jimbo la Oaxaca. Kukamatwa kwa Gortari, Eduardo na Dongyang ulikuwa ushindi mkubwa wa kwanza wa Tume ya Dunia. Ushindi huo ukalipua wimbi la kukamatwa kwa wahalifu wa kimataifa, wa Kolonia Santita, dunia nzima.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kesho yake Ijumaa Rais wa Meksiko alirudi kutoka Panama na aliomba kuonana na Vijana wa Tume; alitaka kuwapongeza binafsi, na kuwapa nishani za heshima kwa mchango wao mkubwa kwa Jamii ya Meksiko. Randall Ortega alilipeleka ombi hilo kwa Rais wa Tume ya Dunia; Rais wa Tume ya Dunia akakaa na Kamati ya Usalama ya Tume ya Dunia na kumrudishia Randall Ortega jawabu, kwamba Vijana wa Tume waliruhusiwa kuonana na Rais wa Meksiko na baadhi ya maafisa wa juu wa serikali ya shirikisho. Saa mbili usiku wa siku hiyo, Ijumaa, kulifanyika sherehe ndogo ya siri nyumbani kwao Debbie; sherehe iliyohudhuriwa na Rais wa Meksiko na mke wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini Meksiko, Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya Nchini Marekani, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu Nchini Meksiko, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, maafisa wa tume na watu wengine wa muhimu katika kazi ya Vijana wa Tume.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Debbie alilia. Alilia kwa nguvu zake zote. Alijua tayari alishampoteza Murphy na yote yale huenda alisababisha yeye. Bila kujuana na Vijana wa Tume huenda wasingepigwa. Debbie Hakukata tamaa. Alikumbuka kitu halafu akamwita dereva. Alimwomba dereva amkimbize Roma Notre haraka ilivyowezekana. Alidhani alijua majambazi walikokuwa wakikimbilia na kuna kitu alitaka kufanya. Dereva akamkubalia na kuondoka kuelekea Roma Notre. Njiani Debbie hakuacha kulia. Aliwaza alivyompoteza Marciano, akawaza kumpoteza na Murphy. Jibu alilolipata ni kumwokoa Murphy kwa gharama yoyote ile.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Polisi wa kituo cha kati cha Coyoacán kumbe hawakuwa mbali na sehemu zile. Walipoona gari zikifukuzana waliona ujanja ni kuwakatisha Vijana wa Tume katika vichochoro. Haikuchukua muda magari sita ya polisi yalitokeza Vallarta (Barabara ya Vallarta) na kuliona gari la Vijana wa Tume Gómez Farías likipepea kwa mwendo mkali kuelekea Cuauhtémoc, na gari za magaidi kwa nyuma yao. Kwa vile Ferrari ilikuwa mbali kidogo na magari ya magaidi, polisi hawakuitilia maanani sana kwa kudhani yale mawili (ya magaidi) ndiyo yaliyokuwa yakifukuzana. Bila kuchelewa, magari mawili ya polisi yalikamata Hidalgo na kuzunguka mpaka Moctezuma halafu yakasimama ghafla katikati ya Moctezuma na Gómez Farías – katikati ya magari mawili ya magaidi na gari la Vijana wa Tume. Wakati huohuo magari mengine (manne) ya polisi yakitokea Mtaa wa Vallarta nayo yakasimama nyuma ya magari ya magaidi; hivyo kufanya magari ya magaidi yawe katikati ya magari ya polisi, na polisi wakaisahau Ferrari ya Lisa.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Wakiwa na suti nzito za kijani na madoa meusi (‘Ghillie Suits’) kwa ajili ya kupigania porini; Vijana wa Tume walikuwa na kofia za chuma, miwani ya kuonea usiku (iliyokuwa na uwezo wa kubinuka chini na juu), redio na mitambo ya mawasiliano migongoni mwao juu ya vizibao vya kuzuia risasi, vitibegi vya msalaba mwekundu (‘Blowout Kits’ – katika mapaja ya miguu yao ya kulia, ndani yake kukiwa na pisto na madawa ya huduma ya kwanza), vitibegi vya kujiokolea (‘Evasion Kits’ – katika mapaja ya miguu yao ya kushoto, ndani yake kukiwa na visu na pesa na ramani ya Meksiko) na bunduki za masafa marefu. Kadhalika, Vijana wa Tume waliamua kuchukua Punisher – waliyoafikiana baadaye kuwa ilikuwa nzuri kuliko RPG-7, ‘Rocket Propelling Gun’, ambayo Mogens alipendekeza waitumie kubomolea Kiwanda cha Dongyang Pharmaceuticals; kwa sababu hakutaka kuleta madhara kwa watu waliokuwa hawana hatia.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Wakati Ford Bronco inatoka katika Kiwanda cha Dongyang Pharmaceuticals S.A de C.V. (kilichomilikiwa na mkurugenzi mkuu wa 'methamphetamine' wa Kolonia Santita mfanyabiashara wa Kichina kutoka Chaling, katika jimbo la Hunan, kusini ya kati ya China, Li Dongyang; na mkurugenzi wa usalama wa Kolonia Santita kutoka Lomas de Chapultepec, Mexico City, Gortari Manuel) Daniel Yehuda na Radia Hosni, waliokuwa wakipiga picha kila kitu kilichokuwa kikiingia na kutoka kiwandani kwa ajili ya ripoti ya upelelezi wao ya baadaye, waliiona. Lakini, hawakujua kama ilikuwa ikienda Varsovia kumuua Murphy na Sajini Mogens.

Bronco ilipofika Varsovia ilisimama kwa fujo mbele ya SUV ya msafara wa Mtoto wa Rais Debbie Patrocinio Abrego, aliyekuwa ndani ya Mgahawa wa Angus akicheza muziki wa 'mariachi' na John Murphy, huku Mogens akilinda usalama wa kamanda wake na usalama wa baa nzima. Kabla majambazi wa Kolonia Santita hawajaleta madhara au fujo yoyote kwa Vijana wa Tume, polisi walifika eneo lile haraka ilivyowezekana! Kwa msaada wa walinzi wa Debbie! Wale majambazi walipekuliwa na kukutwa na bastola moja ya Akdal Ghost, bunduki mbili za AK-47, na picha nne za Vijana wa Tume ndani ya gari yao. Polisi waliwakamata na kuwapeleka katika kituo cha polisi cha Tume ya Dunia kilichopo Zona Rosa, Mexico City.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Vijana wa Tume walipofika kambini chini ya ulinzi mkali wakiwa na Kahima, polisi wengi walionekana kuwapigia saluti lakini wakubwa wao wakawakataza na kuwambia wao walikuwa watu wa kawaida kama wao. Walisindikizwa na lundo la polisi mpaka ndani ya jumba la utawala Murphy alimokuwa ameuhifadhi mwili wa Radia. Walipofika walishtuka, na hata kuwashangaza polisi. Mwili wa Radia haukuwepo! Walitafuta kila sehemu, na kuwambia polisi wawasaidie kutafuta, lakini Radia alishapotea. Murphy alipata wazo na kutoka nje, kwa kukimbia, polisi wengi wakimfuata; mpaka katika helikopta ya DEA ambapo alifungua mlango na kuingia ndani. Ndani ya helikopta hakukuwa na mtu!”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Radia Hosni alikuwa na bahati kuliko watu wote duniani. Frederik Mogens alipofika katika helikopta na kukuta Murphy na Yehuda wakihangaika kuutafuta mwili wa Radia, hakushangazwa na walichomwambia. Kwa sababu alijua nini kilitokea. Radia alikutwa akipumua kwa mbali. Hivyo, Debbie na marubani walimchukua na kumpeleka Mexico City haraka ilivyowezekana. Black Hawk waliyokuwa wakiishangaa ilikuwa ya DEA. Lakini si ile waliyokwenda nayo Oaxaca. Ilikuwa nyingine ya DEA, iliyotumwa na Randall Ortega kuwachukua Vijana wa Tume na kuwapeleka Mexico City haraka ilivyowezekana. Black Hawk waliyokwenda nayo Oaxaca ndiyo iliyomchukua Radia na Debbie na kuwapeleka Altamirano (hospitali ya tume) mjini Mexico City. Mogens angekwenda pia na akina Debbie; lakini alibaki kwa ajili ya kumlinda El Tigre, na mizigo yake, na baadhi ya makamanda wake wachache. El Tigre angeweza kutoroka kama angebaki na polisi peke yao, na Mogens hakutaka kufanya makosa.”
Enock Maregesi, Kolonia Santita

Enock Maregesi
“Kasoro za Uzi zilizofanya zisitumiwe tena na kikosi cha usalama cha rais wa Marekani ni kutokuwa na shabaha imara katika umbali mfupi (hutawanya risasi na huleta madhara makubwa katika umbali mfupi hivyo kuweza kudhuru hata watu wasiokuwa na hatia) na kutokuwa na uwezo wa kutoboa kinga ya risasi dhidi ya magaidi wanaotumia mavazi ya kuzuia risasi, wanaotishia usalama wa rais wa Marekani. Gaidi mwenye mavazi ya kuzuia risasi aliweza kumdhuru rais kwa maana ya USSS kushindwa kumdhibiti. Badala yake, sasa USSS wanatumia FNP90 – zenye uwezo wa kutoboa kinga ya risasi, na ambazo hazileti madhara makubwa katika umbali mfupi na katika umbali mrefu. Bunduki hizi, zenye uwezo wa kubeba risasi 100 katika chemba zake mbili za Kampuni ya Beta ('Century Magazines'), zilitumiwa na magaidi wa Kolonia Santita dhidi ya Vijana wa Tume na dhidi ya polisi wa Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Ghillie ni mavazi yaliyotumiwa na makomandoo wa Tume ya Dunia ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya (Frederik Mogens, Radia Hosni, Daniel Yehuda na John Murphy) kama mbinu ya kujificha kwa kujifananisha na rangi au maumbo ya mazingira ya Msitu wa Benson Bennett, kama afanyavyo kinyonga. Hata hivyo, walivyoingia katika jumba la utawala katika maabara za Kolonia Santita ndani ya Msitu wa Benson Bennett katika mji wa Salina Cruz, Vijana wa Tume walivua suti zao za ghillie; kusudi iwe rahisi kwao kupambana na jeshi binafsi la Kolonia Santita, liitwalo 'autodefensa'.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Vitibegi vya makomandoo wa Tume ya Dunia (vitibegi vya msalaba mwekundu na vitibegi vya kujiokolea) vilikuwa na vifaa maridadi vya kisasa kama vile pisto, visu, madawa ya huduma ya kwanza, kalamu za Inka, ramani za Meksiko, tochi ndogo zenye mwanga mkali za Cyba-Lite, Vioo vya TOPS, vibiriti vya Firesteel, pasi za kusafiria, pesa na vipenga vyenye viwango vya sauti vya desabo 126. Kipenga chenye kiwango cha sauti cha desabo 126 kinaweza kupasua ngoma za masikio ya adui, na kuwajulisha Vijana wa Tume mwenzao alipo hivyo kwenda haraka na kumpa msaada.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“XM29 OICW ni bunduki iliyowasaidia Vijana wa Tume kubomoa jengo la utawala la Kolonia Santita katika Kiwanda cha Dongyang Pharmaceuticals jijini Mexico City, iliyowasaidia kukamata baadhi ya wakurugenzi wa Kolonia Santita kabla hawajatoroshwa na walinzi wao makomandoo. Bunduki hii inayotumia teknolojia ya OICW ('Objective Individual Combat Weapon') iliyotengenezwa na Kiwanda cha Heckler & Koch cha Ujerumani, ina uwezo wa kufyatua makombora ya HEAB ('High Explosive Air Bursting') yenye ukubwa wa milimeta 20; ambayo hulipuka hewani kabla ya kugonga shabaha, kwa lengo la kusambaza vyuma vya moto katika eneo lote walipojificha maadui. Bunduki hizi hazitumiki tena. Zilitumika mara ya mwisho mwaka 2004.”
Enock Maregesi